Kisa Miquissone, Tau, Al Ahly Yavunja Mkataba na Ajayi

 

MABINGWA wa Afrika wenye historia kubwa katika Soka Barani humo, Al Ahly Sc ya Misri imevunja rasmi mkataba na kiungo wao, Junior Ajayi (25) raia wa Nigeria.

Ajayi ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Nigeria, alijiunga na timu hiyo mwaka 2016 akitokea CS Sfaxien ya Tunisina katika msimu wake wa kwanza aliifungia Ahly mabao 12 na assists 7 katika michezo 39 ya mashindano yote ambayo alicheza.

Ajayi amefanikiwa kuchukua mataji 11 tangu ajiunge na Al Ahly ikiwemo Ligi Kuu ya Misri  (mara 4), Egypt Cups (mara 2), Egyptian Super Cups (mara 2), CAF Champions Leagues (mara 2) na CAF Super Cup (mara 1).
Akiwa Ahly amecheza jumla ya mechi-161, amefunga mabao 41 na assist 30.

Majeruhi ya mara kwa mara yamekuwa yakimwandama mkali huyo pamoja na ushindani uliopo Klabuni hapo kutokana na Ahly kumsajili aliyekuwa kiungo wa Simba, Luis Miquissone na Percy Tau kiasi cha Ajayi kukosa kabisa nafasi mbele ya wakali hao.

Tangu msimu umeanza, mbele Kocha Pitso Mosimane, Ajayi hajafanikiwa kucheza hata mchezo mmoja jambo ambalo limewalazimu Ahly kuvunja mkataba wake mapema kabla dirisha la usajili la majira ya joto halijafunguliwa huku ikielezwa kuwa kiungo huyo huenda akatimkia Barani Ulaya.

Previous Post Next Post

Translate